IMECHANGIWA NA SALIM HIMID WA UFARANSA - 8/6/2010
01
Bi . . . mbona kimya
Hata mwisho wa dunia
Wanitatanya na njia?
02
Si mfu, si kiwete
Si Amani, si Kikwete
Nauguwa kwa matete
03
Yote haya ni ya nini
Ya kunikata maini
Pingu, tazitoa lini?
04
Tazama leo na kesho
Juzi, jana, si kopesho
Yetu, sitie komesho
05
Si Mwarabu, si Mzungu
Si Ngezi, si Takaungu
Nimezengwa, zungu zungu!
06
Kutamani si kupata
Funuwa zako karata
Twende kwa Mparapata!
07
Jozani hata Wete
Wapi Chanda, wapi Pete?
Kiza kaandama Kete
08
Vuga, Shangani, Malindi
Sala zetu za vipindi
Si Tanga wala si Lindi!
09
Chakula kiwe mseto
Ngisi, kambare za peto
Biriani ladha beto
10
Kumbuka Tasi na Changu
Wote ni waja wa M'Ngu
Zohali, Zuhura wangu
11
Bi . . ., mbona kimya?
Si karata, si mpira
Nimezongwa na hasira
12
Hasira, ndugu wa Pwete
Ni suhuba wa Uwete
Wa kuketi pwetepwete!
13
Tutambuwe kwa yakini
Tiba ponesha maini
Iwe Taha na Yasini
14
Tufikapo papo hapo
Pasiwe tena mitapo
Tukumbuke Mkapvapvo!
15
Badamu, ndani mwa kungu
Haivunjwi kwa marungu
Agizo la Bwana M'Ngu
16
Yote haya kuyasema
Tuhudumu yalo mema
Na maovu kuyatema!
17
Pasiwe na tese tese
Za Bwanamkubwa Dese
Na kulala wese wese
18
Fensi hii na ya nini
Ya maua vipinini
Na kuuguza maini?
19
Tufikapo tutakapo
Bandarini ndio hapo
Tujivushe na mitapo
20
Abiria chungu chungu
Jahazi yavunja gungu
Joshi, si wingi utungu!
21
Bi . . ., mbona kimya?
Wingi maji, si maziwa
Titi mama, si za ndiwa
22
Ndiwa usibabaike
Na kutaka ujifiche
Tausi dume, ni mke!
23
Tujipambe kwa majuti
Ya kupigia saluti
Kwa tambavu, si makuti!
24
Hapa wino kaukapo
Ndipo tume ituapo
Yangu risala ikomapo
25
Hala hala pendo langu
Upoleze moyo wangu
Niwe wako, uwe wangu!
____________
S. H.
Paris, France
(+336-27146412)
8th of June 2010.
Wednesday, June 9, 2010
Subscribe to:
Posts (Atom)