Nyimbo zifuatazo, ambazo kwa sasa zinapotea tuliziimba katika miaka ya 1960 wakati tukiwa wadogo au tulizisikia zikiimbwa katika hafla mbalimbali kama vile za kuzaliwa watoto, za kukuwa watoto (kufikia balehe), harusini na matangani.
Nilizowahi kuzisikia katika balehe ni kama zifuatazo:
NGWANDINGWANDI
1. Ngwandi ngwandi,
Kanyanyamala mchigoda iyo mwende
Maana yake katika Kiswahili ni:
Huyo huyo aliyekaa kiti kikuu ndiye anayependwa.
Wimbo huu huimbwa baada ya mwali kunema. Anaposhushwa chini, hufikia juu ya magoti ya mnandi/mkasano wake naye ndio humnema tena akiwa chini na huimbwa wimbo huu kama vile kumsifia jinsi alivyopendeza mwali huyo na kuwapa moyo na kuwasifia wazazi waliomlea, na kwa jambo hilo mwali hutunzwa.
MWALI FVIANOGILE
2. Mwali vianogile, mwali vianogile kanoga chitambi chiyafvalile!
Aeee vianogile aeee vianogile kanoga chitambi chiafvalile!
Maana yake katika Kiswahili ni:
Mwali huyu amependeza sana, mwali huyu amependeza kwa nguo alizovaa!
Aeee amependeza kweli aeee! amependeza kwa nguo (kitambi) alizovaa!
Wimbo huu huimbwa kabla mwali hajapandishwa mabegani kunema (mchinhumbili). Yaani baada ya kupambwa wanawake huimba wimbo huu kabla ya mbebaji mwali hajamuinua ili akaneme.
SAKE SAKE
3. Sake sake kunila kwingoma,
Kana umbone sogela kuno (ukiniona sogea huku!)
Eee!
Ahee heeheeheee kana umbone sogela kuno x 2
Wimbo huu sifahamu maana yake mstari wa kwanza. Yaelekea ni wimbo wa shangilizi maalum zinazofanywa na kina mama baada ya kumfunda binti yao. Wanawake waimbapo wimbo huu hukalia magoti na miguu ikiwa nyuma yao, wanavalia kanga tumboni na kuacha maziwa yakiwa wazi na viganja vyao vinapiga chini kutoka usawa kama wa futi moja toka juu. Hivyo sauti inatoka kwa pamoja ya viganja hivyo vinapofika chini kama vile watu wapigavyo makofi. Hufanya hivyo huku wakicheza na kufurahi mwendo wa saa 11 asubuhi kunapokaribia kucha.
CHIDONDOLO
4. Mwali chaajaga choni mwe,
Iyo chidondolo na chilawe! (mara nyingi tu, kutegemea na vya kuonyeshwa)
Tafsiri:
Mwali huwa anakula nini?
Hicho alichokuwa anakula na kitolewe kionyeshwe tukione!
Wimbo huu huimbwa katika hafla maalum iitwayo
Chidondolo. Yaani hafla hii hutayarishwa kama sehemu ya kumtoa mwali. Yaani wazazi wa mwali huyu wanauthibitishia umati wa jamii iliyowazunguka kwamba binti yao amekuwa vile kwa sababu alilishwa vyakula vituatavyo. Vyakula hivyo ndio vinavyoonyeshwa katika hafla hii. Vyakula hivyo zaidi zaidi huwa ni mboga mbalimbali, kuku, mayai, nafaka; kwa jumla jinsi mzazi atavyoweza kuvikusanya vyakula vya kawaida vya sehemu ile. Kila kimoja kinaonyeshwa tofauti kisha vyakula vile kila aliyehudhuria huchukua kimojawapo au hupikwa kwa ajili ya wageni waliohudhuria.
ZA HARUSINI
5. Kwereza mikwambe kwerezaa
na miti mikulu tule nyama.
Huu ni wimbo wa Kiswahili uliokuwa ukiimbwa sana kwenye harusi kama sehemu ya shangilizi. Inaelekea hii mikwambe huenda ikawa ni kitu kilichokuwa kikitumiwa katika muziki wa asili. Kwa sababu kwereza maana yake ni kama kuvuta kwa madoido.
CHIKUWIII
6. Chikuiiiiii kodeng'ela mchanya chikuiiii! Kodeng'ela mchanya!
Tafsiri:
Chikui ni aina ya ndege/mnyama mdogo. Mnyama huyu hucheza juu ya miti. Hivyo tafsiri ya wimbo huu ni kumsifia huyu Chikui kwamba huchezea juu!
Wimbo huu ni wa ngoma aina ya
Kigoma. Kigoma ni ngoma ya wanawake watupu. Ngoma hii huchezwa na kinamama usiku kucha wakati wa shughuli ya kufunda mwali wakiwa ndani. Uchezaji wake ni vyovyote vile utakavyo, ikiwa wima au umekaa na kwa vigelegele kwa wingi sana.
JISIKIE FAHARI KUWA WEWE NI MTANZANIA !!!
7. Wee imwana seke ulile gwee!
Kwa Mtanzania,
Mwanangu seke ulile gwee!
Kwa Mtanzania!
Tafsiri:
Mwanangu wala usisikitike(usilie!)!
Wewe ni Mtanzania x zozote.
Wimbo huu uliimbwa wakati wa shangilizi na ulikuja kuimbwa baada ya Muungano wa Tanganyika na Unguja mwaka 1964. Wimbo huu ulikuwa ukitangaza kujidai kwa wenye nchi kwamba hakuna sababu ya kusikitika wala kuwa wanyonge kwa sababu sisi ni Watanzania (ni sifa kubwa sana kuwa Mtanzania). Ni wimbo wa kujivunia uzalendo wa Watanzania.
8. Eeeeeh Namchua nie! x 2
Kondemela iwana ngalila kwani,
Miago sina mtumba na mchuwa!
Tafsiri:
Mimi ni yatima, mimi ni mkiwa!
Unaniachia watoto niwapeleke wapi,
Mimi sina Mjomba(Mwangalizi) ni mkiwa!
9. Na mchuwa mie, eeeeh, na mchuwa mie noilolesa,
Niwe na baba, niwe na mama asongelele chiti chitali sawasawa na Ulanga,
Eeeeh noilolesa.
Tafsiri:
Mimi ni mkiwa, mimi ni mkiwa nimejikunyata,
Ningekuwa na baba na mama, wangenitengenezea kiti (samani) zing'arazo kama ulanga
nimejikunyata!
10.
Pwaga mulile gwe, Kwa sulutani x2
Tafsiri: Sasa umekuwa sultani (umekuwa mtu mzima!)
Huu ni wimbo wa ngoma ya VIJEMBE. Vijembe ni ngoma iliyokuwa ikichezwa na wanaume wakati wa kuwakaribisha vijana waliotoka jandoni. Vijembe hivi vilikuwa vikipigwa na kutoa sauti na wanaume hawa wakiwa wima walikuwa wakiimba wimbo huu wakiwa katika duara. Wimbo huu uliimbwa kumpongeza aliyetoka jandoni kwamba sasa ameshakuwa mtu mzima wa kutegemewa (kama sultani). Yaani ameshakuwa mtu mzima baada ya kutoka jandoni maana amefundishwa namna ya kujitegemea.