| Wananchi wa kabila la wandorobo wakiwa kwenye mkutano wakati wakiongea na mwandishi wa makala haya hayupo pichani katika Kitongoji chao | | ‘Hatutaki kuitwa Wandorobo, sisi ni Akiyee…ndorobo ni mdudu anayeng’ata ng'ombe na kuambukiza magonjwa ya nagana,” anasema Olonyoiki Lotiengo. Akiyee maarufu kama Wandorobo ni kabila dogo miongoni mwa makabila yanayoishi katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara. Makabila mengine yaliyopo kwenye wilaya hiyo ni Wapare, Wachaga, Wamasai, Wanguu, Warangi na Waarusha. Makabila hayo hujishughulisha na kilimo, ufugaji, pamoja na biashara ndogo. Jamii ya kabila hilo dogo la Akiyee katika wilaya hiyo, linaishi katika vijiji vya Kitwai A, Kitwai B, Komolo, Loiborsoit B, Loborsiret na Lormorjoi. Jamii hiyo ni kabila dogo ambalo lina jumla ya watu 188, ambapo ni sawa na asilimia 0.11 ya wakazi wote wa wilaya hiyo, ambao ni 172, 660. Jamii hiyo haina tofauti na jamii ya Wahazabe (Watindiga), wanaoishi katika eneo la Yaenda Chini wilaya ya Mbulu, kwani maisha yao ni ya kuhama hama kutoka eneo moja hadi eneo jingine ili kutafuta chakula na maji. Kabila hilo la Akiyee huishi kwa kutegemea kurina asali, mizizi ya miti, matunda pori na wanyama pori kama vyakula vyao vikuu. Pia, jamii hiyo haina desturi ya kuhudhuria katika zahanati, kituo cha afya au hospitali kwa ajili ya kupata matibabu ya maradhi. Hata wajawazito wanaotaka kujifungua, hutumia dawa za asili zitokanazo na miti mbalimbali kwa ajili ya kujitibu. Olonyoiki Lotiengo ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lormorjo Kijiji cha Lormorjoi. Anaeleza kuwa kitongoji chake kina wananchi 55 ambao umri wao umeanzia miaka 30, na hakuna mwananchi mwenye umri chini ya miaka hiyo. Kitongoji hicho kipo katikati ya pori, lenye msitu mnene na kimejitenga na vitongoji vingine katika Kijiji cha Kitwai B. Kipo umbali wa kilometa 30 kutoka makao makuu ya kijiji hicho na umbali wa kilometa 100 kutoka makao makuu ya wilaya hiyo. HabariLeo ilifika katika maeneo hayo na kujionea hali halisi ya maisha ya jamii hiyo, ambayo ipo hatarini kutoweka kutokana na jamii hiyo kushindwa kuongezeka, kutokana na sababu mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo hali ngumu ya maisha yanayowakabili wananchi hawa. Kitongoji hicho hakina huduma za maji, yaani visima vilivyochimbwa na wananchi hao na serikali, bali hutumia visima vya asili ambavyo wamevikuta. Wanadai huenda visima hivyo vimewekwa na Mungu wakati akiumba dunia. Visima hivyo vipo katikati ya miamba ya mawe. Pia, katika kitongoji hicho hakuna hospitali, kutokana na jamii hiyo kutumia zaidi dawa za miti shamba wakati wakiugua magonjwa mbalimbali, ikiwemo wanawake wanaojifungua. Katika kitongoji nilishuhudia kuwepo kwa wanyama aina ya mbwa pekee, na hakuna mifugo kama ilivyo kwenye vijiji vingine. Hali hiyo ilielezwa ni kutokana na hali ya umasikini, unaoikabili jamii hiyo. Ni pia katika hali isiyo ya kawaida, kuikuta kwenye nyumba za Watanzania ni kutokuta mtoto mdogo. Hali hiyo ilinishtua kidogo, kutokana na kuzoeleka kuwa Watanzania tumebarikiwa kuwa na watoto wengi, hususani katika maeneo ya vijijini. Hali ni tofauti katika kitongoji hiki, kwani hakuna watoto. Hiyo ni wazi kuwa hakuna shule yoyote ya msingi hata ya awali. Shule ya msingi ipo umbali wa kilometa 30 kutoka kwenye kitongoji hicho. Jamii hiyo hivi sasa imebadilika na huvaa nguo kulingana na mavazi yanayovaliwa na jamii ya Wamasai. Jamii hiyo inasikilizana na Wamasai, kutokana na kuzungukwa na kabila hilo kwa eneo kubwa na pia kutokana na kulitegemea katika maisha yao. Katika mazungumzo yetu na Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, nililazimika kupata mkalimani ambaye ni mzee wa mila wa jamii ya Wamasai wa Kata ya Kitwai A, Wiliam Moringe. Moringe alikuwa akitafsiri kwa Kiswahili maelezo yaliyokuwa yakitolewa na mwenyekiti huyo wa kitongoji, ambaye alikuwa akizungumza Kiswahili katika maeneo machache. Mwenyekiti huyo anasema wanaishi kwa kutegemea rehema za Mwenyezi Mungu, kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili hivi sasa, kutokana na ukame uliopo katika kitongoji chao. Ukame umesababisha maji waliyokuwa wakiyategemea kutokana na mvua, kuanza kukauka. Kutokana na ukame huo wanalazimika kuponda mizizi wanayoiita ‘Kisherembwa’. Huitumia mizizi hiyo kama maji, kutokana na mizizi hiyo kuwa na maji mengi. Pia hutumia mizizi hiyo kama chakula. Kutokana na ukame huo, pia matunda aina ya “Ndungu’ waliyozoea kula kama chakula chao, yanaanza kukauka huko porini. Hali hiyo imeanza kuleta njaa kali katika jamii hiyo. Anasema katika kukabiliana na maradhi mbalimbali kulingana na mazingira wanayoishi, jamii hiyo imekuwa ikitumia dawa mbalimbali katika kutibu maradhi yao. Anataja miti ya dawa wanazotumia pamoja na magonjwa wanayotibu. Mti wa ‘Mukutani’ ni dawa ambayo wanatumia kwa ajili ya maradhi ya minyoo, tumbo na kuondoa nyongo mwilini. Mti huo hupondwa na kisha kunywa maji yake na kufanya utapike nyongo, pamoja na kuua minyoo tumboni. Mafuta ya mti wa ‘Ndemwee’ ambayo hutumika kwa kuchanganya na asali, ni dawa ya kutibu maradhi ya kifua. Mti wa ‘Singwai’ hutumika kutibu maradhi ya tumbo na kuzuia kuharisha na mti wa ‘Osiamali’, hutumika kama dawa ya kutibu maradhi ya tumbo. Dawa zingine za miti shamba ni ‘Sogonoi’ ambao huutumia kama dawa ya malaria, homa na tumbo. Mizizi ya jamii ya Olduvai hutumika kama dawa ya magonjwa ya zinaa. Pia jamii hiyo huwa inajiburudisha kwa kutengeneza pombe yao ya kienyeji, inayotengenezwa kwa asali. Pombe hiyo inaitwa ‘huumi’ na hutumika zaidi katika sherehe mbalimbali wanazozifanya kijijini hapo. Dawa nyingine walizo nazo ni za kujipaka kuepuka madhara ya wanyama wakali. Anaeleza kuwa dawa hizo ni za kusahaulisha ama kupoteza eneo ambalo mtu anataka kufika, na pia zinaweza kumsafirisha bure katika vyombo vya usafiri. Anataja dawa hizo kuwa ni Mberesero na Ormudee. Anasema dawa hizo unaweza kuzitumia, kwa kuchoma moto na kisha kuzungushia majivu yake mahali ulipo, ama kuzitwanga na kuweka mdomoni ili kila unayezungumza naye, akubaliane na wewe jambo lolote. Inadaiwa kuwa dawa hizo, hutumiwa na majangili wakati wanapokwenda kuwinda wanyama kwenye misitu ya hifadhi, na kujizungushia dawa hizo na kushindwa kuonekana na askari wa hifadhi hizo, huku majangili yao wakiwaona askari hao. Hata hivyo, jamii hiyo imeshindwa kuongezeka kutokana na mila na desturi potofu, ambazo pia zinachangiwa na hali mbaya ya uchumi. Baadhi ya mila hizo ni mwanamke wa jamii hiyo anapopata ujauzito, anajitokeza mwanaume wa jamii ya Wamasai na kujitolea kulea mimba kwa kutoa ng’ombe, ili endapo atazaliwa mtoto wa kike basi atalazimika kuolewa na mfugaji huyo. Kutokana na utaratibu wa wanawake kuozwa kwa kabila ya kifugaji ili kupata mifugo, imekuwa vigumu kwa vijana wa kabila hilo kupata mwanamke wa kuoa, hivyo idadi yao kuzidi kupungua. Katika kuisaidia jamii kuondokana na maisha magumu, serikali ya wilaya hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa jamii hiyo, kulingana na mahitaji yao. Serikali ya wilaya hiyo ilitoa msaada wa mizinga ya kisasa 60 na vifaa vingine vya ufugaji wa nyuki, vyenye thamani ya Sh 1,200,000. Serikali kuu pia ilitoa mizinga yenye thamani ya Sh 1,920,000 katika kipindi cha miaka ya nyuma. Jitihada zaidi za serikali, zinatakiwa kutumika katika kuikomboa jamii hiyo ambayo inazidi kutoweka, ikiwa ni pamoja na kuwaweka mahali pamoja ili kuweza kuwapatia huduma mbalimbali za jamii ili waachane na dhana ya kuhama hama. Hatua hiyo itasaidia jamii hiyo, kuondokana na umasikini hivyo kuanza kulima na kujipatia kipato. |
No comments:
Post a Comment
BLOGU YA KUWEKA KUMBUKUMBU ZA ASILI ZA WATANZANIA, WAAFRIKA NA WOTE WAZUNGUMZAO LUGHA YA KISWAHILI DUNIANI.