Sunday, February 28, 2010

MOLA MBARIKI MAMA (SHAIRI)

LIMECHANGIWA NA NASRA MOHAMED WA ZANZIBAR
28.2.2010.

M O L A M B A R I K I M A M A

Ya Rabbi Mola Rahima, mwenye kumiliki enzi,
Pokea yangu kalima, ewe usiye na mwezi,
Dua langu nalituma, kwa usiye ni vikwazi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Mola mbariki mama, kwa yake bora malezi,
Lolote nitalosema, halitoshi kumuenzi,
Alivyonilea vema, na kunifuta machozi
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Amenifunza hekima, vipi niishi na wenzi,
Na pia bora heshima, nisifate wapotozi,
Hii ni kubwa neema, gizani huwa kurunzi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Nilipopigwa na homa, udogoni hizo enzi,
Mama kucha husimama, kwa ule wangu ulizi
Kwa zake nyingi huruma, humiminikwa machozi.
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Kumbatio lake mama, lilinipa utulizi
Kwa sauti yake njema, aliniimbia tenzi
Na kunifunza kusema, mie wake mwanafunzi
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Alinilaza kwa hima, niwapo na usingizi,
Japo awe anahema, kwa kuzidiwa makazi,
Hakika zake huduma, ni pendo lililo wazi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Ni nini nimpe mama, kulilipa lake penzi,
Dhahabu kama mlima, ibebwe na wachukuzi,
Haitoshi ninasema, kwa huyu mwema mzazi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Beti hii nasimama, bila kufanya mapozi,
Machache niliyosema, mama kumpa pongezi,
Hakika yake karama, kuisahau siwezi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi.

Saturday, February 20, 2010

UTENZI WA WALYD K. HASSAN, DR. YUSSUF S. SALIM, AMANI A. KARUME & MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD

Umeandikwa na Salim Himid (bwanatosha@hotmail.com)
Subject: UTENZI wa Walyd K. Hassan, Dr Yussuf S. Salim, Amani A. Karume & Maalim Seif Sharif (Sehemu 1, 2 & 3)
Date: Wed, 20 Jan 2010 18:39:34 +0000

Sehemu Ya Kwanza

01)-King Walyd mwana wetu
Dokta Yussuf nakwambia
Si mtoto "petu petu"
Lako bora kusikia
Hata uliza Sepetu
Usije potea njia!

02)-Usije potea njia
Wala kupiga mateke
Na kuchanua mikia
Ukapambwa na upweke
Bora tega "kia kia"
Zanzibar isitoweke!

03)-Zanzibar isitoweke
Tutafute itifaki
Du'a zetu tupeleke
Ha Pateli nae Fakih
Mwenye Enzi ndo Mpweke
'Ridhiano kubariki!

04)-'Ridhiano kubariki
Moyo mwema ndio chambo
Pia hayo tusadiki
Tupate kuona mambo
Ifikapo yetu Iddi
Tusije tokwa machango!

05)-Tusije tokwa machango
Angamiza roho zetu
Bora tubane mibango
Kuhifadhi kilo chetu
Amani awe mlango
Na Sefu ndo wimbi letu!

Sehemu Ya Pili

06)-Abdallah Hashim wauzisa
"Blekie bado hajapita?"
ZIRPP, MUWAZA, sisitiza
Sote tusipigwe mateke!

07)-Sote tusipigwe mateke
Yetu zanzibar sitoweke
Zarina, Karama, watete
Naila Majid ndo Rubani!

08)-Naila Majid ndo Rubani
Alipoonja MAGEUZI
Kutuambia tusidhani
Zanzibar ni Kilombero!

09)-Zanzibar si Kilombero
Twache kutiana kero
Yuwapi wetu ndugu Hero
Aje tuvalisha visutu?

10)-Aje tuvalisha visutu
Chankiwiti na mrututu
Farouku nae kuthubutu
Warembo wote kuwavisha!

Sehemu Ya tatu

11)-Yote haya kuongea, kweli ndipo isogee
Ndugu hatujapotea, amani naitokee
Kupenda Zenjibaria, mahaba tutegemee!

12)-Mahaba tutegemee, tusitoswe baharini
Wataka tutokomee, Makamba na mahaini
Msekwa naasekwekwe, 'Ridhiano kubaini!

13)-'Ridhiano kubaini, Miwafaka kwenda pogo
King Hassan haamini, ona watu kwa kisogo
Amani, Sefu, kwa nini, mwatupikia mikogo?

14)-Mwatupikia mikogo, Jussa kuchana viatu
Na tule wetu mhogo, Kikwete apige patu
Amani isende pogo, Zenjibari ina watu!

15)-Zenjibari ina watu, wenye yao tarbia
Uswahili ni ubantu, pamoja na Arabia
Ngazija nao si chatu, Uhindi na Somalia!

Wakatabahu bi-l-yadii,
Salim H. Bwanatosha
(Mngazija wa Zanzibar/Mzenjibari wa Komoro)
Paris, France (+336-27146412)



27
Sefu kupandisha gia
Amani nae kaingia
Wawakilishi wakamavamia
Tulobaki ndo "songa mbele"

28
Tulobaki ndo "songa mbele"
Tujionee ya mabele
Ya Zanzibar hata Mkele
Undugu ndo uwe Jahazi

29
Undugu ndo uwe Jahazi
Kupanda Kusi na Kaskazi
Tusije fanywa wajakazi
Wa majambazi mambo leo

30
Wa majambazi mambo leo
Nchi kufanywa kitoweo
Siasa kuwa ndo uteo
Kuhifadhi yao majungu

31
Kuhifadhi yao majungu
Bila ya kujali M'Ngu
Nchi oneshwa matungu
Rehema itapo wadia?

32
Rehema itapo wadia
Tusiogope kuingia
Tujue yalobakia
Wanaume na wanawake

33
Wanaume na wanawake
Pasiwe alo peke yake
Kula mtu apewe chake
Mseto, choroko na wali

34
Mseto, choroko na wali
Ngoma huchezwa kwa ndzumari
Ndio kuchuma yote mali
Ukweli usiwe na miko

35
Ukweli usiwe na miko
Jinsia iwe hadi mwisho
Kwetu, ungwana ndo mwito
Zanzibar kupandishwa juu

36
Zanzibar kupandishwa juu
Shamhuna hana makuu
Atajipamba Siku Kuu
Na Khatibu kushangiria


37
Na haya yote tunosema
Magazetini tunagema
Fununu papo zinatema
London mkutanoni twende

38
London mkutanoni twende
Tukafichuliwe ya mende
Yasemwao ndani na nde
Maridhiano yawe wazi

39
Maridhiano yawe wazi
Ukweli upate malazi
Kwa Kusi na Kaskazi
Ndo wananchi watakavyo

40
Ndo wananchi watakavyo
Wawakilishi watakayo
Ya kuridhisha Mba Chao
Kwa vishindo na vuguvugu

41
Kwa vishindo na vuguvugu
Tulaani ukorofi sugu
Tupate kufyeka magugu
Kwa kupanta jaha ya tija!

Rendez-vous Abbey Schhol Leisure Centre, Woodbridge Road
Barking, East London
Jumamosi, 13/02/10.

42

Mkutanoni Landani

Sefu keta wake ndani

Kawambia "Ikhiwani

Tusahau yalopita"



43

Tusahau yalopita

Amani mshinda vita

Zanzibar inatuita

Tujihodari kwa yote



44

Tujihodari kwa yote

Tusikose kote kote

Visiwa ni vyetu sote

Tumlaani Shetani!



45

Tumlaani Shetani

Tukinge wetu Watwani

Tujijue sisi nani

Tusitupe Mba Chao



46

Tusitupe Mba Chao

Kwa msala upitao
Shime tuyajue hayo

Zanzibar ipande juu



47

Zanzibar ipande juu

Wirathi wa Mwinyi Mkuu

Pujini hata Bwejuu

Pasiwe waasi tena



48

Pasiwe waasi tena

Mashekhe wamesha nena

Tuhifadhi yalo mema

Tuache ya maferembwe



49

Tuache ya marefembwe

Suluhisho si bwebwe mbwe

Tupanie kwa vibombwe

Ndo chetu kuwa halisi



50

Kuwa na chetu halisi

Kisichokuwa rahisi

Historia yatukisi

Ridhiano ndio ngao



51

Ridhiano ndio ngao

Sote na tujue hayo

Tunapo pambana nao

Wanapopika majungu



52

Wanapopika majungu

Kututia zungu zungu

Kukana amri za M'Ngu

Tunyakue yalokita



53

Tunyakue yalokita

Kwa kujikinga na vita

Mchakato sije sita

Tarakhe kusonga mbele



54

Tarekhe kusonga mbele

Uhai usona ndwele

Sawahil hata Mkelle

Zenjibari ndo johari



55

Zenjibari ndo johari

Wimbi letu la bahari

Iwe ndo kwetu fahari

Ya kucheza mtu kwao



56

Ya kucheza mtu kwao

Aje tunzwa kwa vipao

Tutapike sumu zao

Nchi tena iwe huru



57

Nchi tena iwe huru

Uungwana kuamaru

Muungano uwe nuru

Tujadidi mikataba



58

Tujadidi mikataba

Pwani pamoja na Bara

Tusizongwe na madhara

Tanzania ijiunde



59

Tanzania ijiunde

Bila ya kuliwa kunde

Kwa heshima tuitunde

Uwe muungano wa kweli



60

Uwe muungano wa kweli

Kama bahari na meli

Daftari na jaduweli

Karume na Sefu hawo!

Wakatabahu,

S. H. M. Bwanatosha

London

Jumapili, 14/02/10