Sunday, February 28, 2010

MOLA MBARIKI MAMA (SHAIRI)

LIMECHANGIWA NA NASRA MOHAMED WA ZANZIBAR
28.2.2010.

M O L A M B A R I K I M A M A

Ya Rabbi Mola Rahima, mwenye kumiliki enzi,
Pokea yangu kalima, ewe usiye na mwezi,
Dua langu nalituma, kwa usiye ni vikwazi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Mola mbariki mama, kwa yake bora malezi,
Lolote nitalosema, halitoshi kumuenzi,
Alivyonilea vema, na kunifuta machozi
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Amenifunza hekima, vipi niishi na wenzi,
Na pia bora heshima, nisifate wapotozi,
Hii ni kubwa neema, gizani huwa kurunzi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Nilipopigwa na homa, udogoni hizo enzi,
Mama kucha husimama, kwa ule wangu ulizi
Kwa zake nyingi huruma, humiminikwa machozi.
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Kumbatio lake mama, lilinipa utulizi
Kwa sauti yake njema, aliniimbia tenzi
Na kunifunza kusema, mie wake mwanafunzi
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Alinilaza kwa hima, niwapo na usingizi,
Japo awe anahema, kwa kuzidiwa makazi,
Hakika zake huduma, ni pendo lililo wazi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Ni nini nimpe mama, kulilipa lake penzi,
Dhahabu kama mlima, ibebwe na wachukuzi,
Haitoshi ninasema, kwa huyu mwema mzazi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi

Beti hii nasimama, bila kufanya mapozi,
Machache niliyosema, mama kumpa pongezi,
Hakika yake karama, kuisahau siwezi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi.

No comments:

Post a Comment

BLOGU YA KUWEKA KUMBUKUMBU ZA ASILI ZA WATANZANIA, WAAFRIKA NA WOTE WAZUNGUMZAO LUGHA YA KISWAHILI DUNIANI.